Kuna mambo mengi ambayo unaweza kuyafanya bila mtaji kabisa na mengine ambayo unaweza kufanya kwa kutumia mtaji mdogo sana ambao nirahisi kupatikana. Hapa nimejaribu kuchambua baadhi tu ya mambo ili kukupa mwanga, nimeangalia mambo ambayo kiuhalisia yanawezekana katika mazingira yatu.
Kitu cha muhimu hapa kabla ya kuanza biashara yoyote ni kuangalia mazingira yako, angalia kama wazo lolote la biashara ambalo unalo kichwani linawezekana katika mazingira yako. Kama haliwezekani basi usikomae nalo sana, angalia linalowezekana katika mazingira yako na anza na lo hilo.
Nilichoandika hapa ni mifano michache kutokana na tafiti nilizofanya mimi, fanya tafiti zako na chukua mifano hii iweke katika mazingira yako kisha ifanyie kazi. Mifano ni mingi sana, fursa ni nyingi sana ambazo siwezi kuziandika zote, tumia mifano hii kama kitu cha kukuzindua kuangalia fursa zinazokuzunguka, jiongeze.
(1) BIASHARA YA KUUZA NGUO
Biashara ya nguo ni moja ya biashara ambazo binafsi naamini ni rahisi sana kuanzisha, hii inatokana na ukweli kuwa kila mtu anahitaji kuvaa na kustirika na kila siku mitindo mipya ya nguo hujitokeza. Unaweza kuanzisha biashara hii kwa kutumia njia karibu zote nilizozitaja hapo juu.
Unaweza kuanzisha kwa kutumia sample, hapa unaweza kununua nguo chache na kuzipitisha kwa majirani zako kuwaonyesha, kupitisha maofisini na kuweka kwenye mitando ya kijamii. Watu watakapoweka oda basi ukaenda kuwanunulia na hapo utakuwa mwanzo wa biashara yako.
Lakini pia unaweza kuwa dalali wa nguo, wa kutafuta wateja kwaajili ya duka flani kwa kuweka nguo zao katika mitando ya kijamii, kutengeneza vipeperushi na kila mtu anaponunua kupitia wewe ukapata kamisheni. Nguo pia unaweza kuziuza kupitia mitando ya kijamii tu, kwa kutengeneza duka lako huko na wewe kuwa kama muuzaji.
Kama nilivyokwisha sema huko awali watu wanaweka oda na kulipia kabla. Hivyo unaweza kuanzisha ukurasa maalum katika mitando yako ya kijamii, ukaipa jina biashara yako na hata kuanzisha blog ambayo utakuwa ukitundika nguo mbalimbali, bei zake na mawasiliano yako.
Hapa watu wakawasiliana na wewe, wakaoda nguo na wewe kuwapelekea majumbani mwao, vyuoni, maofisini au kuwatumia kwa njia za mabasi. Unaweza kuuza nguo, viatu, mikoba, mabegi, mikanda, pochi manukato, mashuka na vitu vingine vingi kwa njia hii na kufanikiwa.
Unaweza kuanza hivi ukiwa na malengo ya kukua mpaka kumiliki duka lako mwenyewe la nguo, au kubakia kuwa muuzaji wa nguo katika mitandao, yote haya yanawezekana ingawa ni muhimu mwisho wa siku kuwa na malengo ya kumiliki ofisi, sehemu ambayo wateja wako wanaweza kukupata wakiwa na matatizo.
Biashara ya nguo ambayo umeianzisha kwa kuzungusha nguo chache za mifano katika maofisi, umeianzisha kwa kuweka picha tu katika mitandao ya kijamii unaweza kuw ana malengo ya kumiliki duka kubwa la nguo, mini shopping mall au shoping mall kabisa, kitu cha muhimu nikuwa na malengo mazuri.
(2) BIASHARA YA KUUZA SIMU ZA MIKONONI
Hii ni biashara nyingine ambayo unaweza kuianzisha hapo ulipo. Unaweza kuanza kwa kuuza sample za simu, kwa mfano kama una simu nzuri unaweza kuanzia hapo. Jitambulishe kwa marafiki zako na watu wako wa karibu kama muuza simu hata kama hujawahi kuuza simu.
Mtaji wa simu unaweza kua mkubwa kidogo, hasa kama utataka kutumia njia ya sample, kwa maana watu watataka waone. Hapa ndipo unaweza kuanza kwa kusambaza sample za vitu vidogo au kuuza vitu vidogo vidogo, kama vile chaja za simu, power bank na makasha ya simu.
Ukianza kuzungusha vitu hivi moja kwa moja watu watahisi unajishughulisha na simu na hapo ndipo utawaambia biashara yako. Download picha za matoleo mapya ya simu, au nenda kabisa kwa wauzaji wa simu wa jumla na piga picha simu au chukua vipeperushi kisha anza kujitangaza.
Tumia mitandao ya kijamii kuweka picha za simu na bei zake, anza kuuza kwa marafiki zako. Unaweza pia kuanza biashara hii kwa kuwa kama wakala wa brand flani ya simu, wafuate na kuwaomba vipeperushi na picha kisha anza kutafuta wateja, anza kwa marafiki zako, ndugu zako, wafanyakazi wenzako na katika mitando ya kijamii.
Ukiweza kuwashawishi wateja na kuuza simu mbili tatu wanaweza kukuamini kama wakala wakakutumia kujitangaza na kuuza simu zao kupitia wewe. Nguvu yako ya ushawishi ndiyo itaweza kukusaidia hapa kuweza kupata wateja wengi na kutengeneza pesa zaidi lakini pia kuweza kuaminika na wauzaji halisi wa simu.
Unaweza kufungua kakibanda kadogo na kuweka vifaa vidogo vidogo vya simu ambavyo havihitaji kabisa mtaji mkubwa, unaweza kuanza kutangaza simu yako mwenyewe, kuwaonyesha marafiki zako na kujitangaza kama muuzaji wa simu.
(3) BIASHARA YA KUUZA CHAKULA
Anza kwa kupika vitafunwa na kuviuza kwa majirani wanaokuzunguka. Kama unajua kupika chapati nzuri, vitumbua, maandazi na vitu vingine kama hivyo basi anza kwa kupika na kuwauzia majirani. Hii ni fursa kubwa kwani ni watu wachache sana hupika vitafunwa asubuhi, wengi hununua.
Pika vitafunwa vyako vizuri na vifunge kwa usafi kisha anza kusambaza kwa majirani asubuhi. Vipaki vizuri ili kuwa tofauti na yule ambaye hupeleka katika duka la jirani, huku ukiongeza ubunifu wa uwapelekea watu asubuhi majumbani mwao. Kwa maana kuwa usisubiri watu kuja kuchukua pika na sambaza majumbani.
Unaweza kuvipaki katika makundi, kwa mfano kundi la vitafunwa vya shilingi mia tano, elfu moja na kuendelea. Hii inamlazimisha mnunuzi kununua vingi na kubwa zaidi vinakuwa katika vifungashio vizuri na visafi ambavyo vitamvutia mlaji.
Huu kwako ni mwanzo, peleka chakula maofisini, kuna ofisi ambazo hupikia watumishi wao chakula na nyingine hazifanyi hivyo, pika chakula cha sample weka fungasha vizuri kisha wapelekee ofisini kuonja kwaajili ya kuweka oda ya chakula chenyewe, kama ni kizuri na hawapikiwi nina uhakika utapata wateja wakuweka oda.
Usiishie tu kuwaza kuuza chakula cha mgahawa, jipanue kuwaza kupika kwenye sherehe. Kuna sherehe nyingi ambazo huandaliwa, jitangaze kama mpishi, peleka sample kwa kamati za sherehe kuwaonyesha chakula chako, tengeneza vipeperushi na wapelekee.
Anza kujitangaza katika mitando ya kijamii. Kwa maana kuwa tafuta jina la biashara yako na anza kulitumia katika mitando ya kijamii kutangaza huduma unazotoa. Unaweza kusema unapokea tenda za chakula maofisini, watu binafsi, sherehe na matukio mbalimbali. Pika chakula chako na piga picha kisha kuwa unaziweka katika mitandao ya kijamii.
Hapa nashauri usiweke picha feki bali picha za chakula unachopika wewe. Huhitaji kupika vyakula vingi na kuvipiga picha bali unaweza kupika chakula cha nyumbani kwako tu na kukipiga picha. Nikimaanisha kuwa kila unapopika chakula kipakue vizuri piga picha na zikusanye kwaajili ya matangazo.
Kwa mfano kama leo umepika wali kuku, upike vizuri, upakue vizuri na upige picha, ukipika ugali fanya hivyo hivyona vyakula vingine. Tengeneza profile ya vyakula na itumie kujitangaza, chapisha vipeperushi vya vyaula vyako na tangaza kwa watu, katika mitando na makundi ya Watsapp.
Kwa maana hiyo katika wazo hili unaweza kuwa na malengo ya kufungua mgahawa ambapo utaanza kwa kupikia watu wakaribu na maofisi ya karibu, lakini pia ukawa na malengo ya kufungua kampuni kwaajili ya kupika kwenye matukio ambayo utajitangaza kwenye sherehe na matukio mbalimbali kupitia mitando ya kijamii au ukafanya vyote kwa pamoja.
Lakini pia unaweza kufanya vyote kwa pamoja. Unaweza kutumia njia ya sample, ukawa dalali wa kampuni ya kupika vyakula katika sherehe kwa kuwatafutia shughuli za kupika, ukawa unapika bites na kuzisambaza katika mashule na mtaani, lakini pia ukapika chakula na kuuza kando kando za barabara nyakati za usiku.
Kwa watu walio mijini ni jambo la kawaida kukuta vyakula vinauzwa pembeni mwa barabara nyakati za usiku. Hii ni biashara ambayo ni rahisi na unaweza kuifanya na haihitaji mtaji mkubwa. Unaweza kupika chips, mishikaki na vyakula vya kawaida, hapa unachohitaji ni kupata eneo ambalo watu wengi hupita mara kwa mara.
No comments:
Post a Comment