By Diana Morsad
Uzoefu unaonyesha kuwa biashara nyingi zilizoanzishwa na wafanyakazi ambao wakati mwingine huwa na elimu ya biashara hufa mapema au hufanya vibaya kwa muda mrefu.
Wapo wafanyakazi huingiza fedha nyingi kwenye biashara na kuishia kukata tamaa kujiingiza kwenye biashara.
Wakati yako masomo mengi ya biashara yanayofundishwa darasani, ukienda kufanya biashara kwa vitendo utagundua kuna elimu nyingine ya biashara inayopatikana huko mtaani haiko kwenye vitabu vyovyote ulivyovisoma na kutunukiwa cheti ulichonacho.
Elimu hii ya mtaani huwa haipatikani bure, kuna gharama zake pia, ingawa gharama hizo huwa hazionekani moja kwa moja. Gharama hizo ni pamoja na kupata hasara, kupoteza muda kubadilisha biashara mara kwa mara na wakati mwingine hata msongo wa mawazo.
Baadhi ya makosa ambayo wafanyakazi huyafanya wanapoanzisha biashara zao ni haya yafuatayo:
Kuanzisha biashara wasizozijua
Unakuta watu wamekaa wanasema biashara ya kuuza chakula inalipa sana, unaona wateja walivyo wengi pale kwa mama Ashura. Wote hawa wanaoshauriana hawajawahi kuwa na biashara kama hiyo na wala hawajui undani wa biashara yenyewe. Mara utasikia mmoja wao anataka kufungua biashara kama hiyo.
Kabla ya kuanzisha biashara ni vyema sana ukatumia muda wako kujifunza hiyo biashara hususani kutoka kwa wanaoifanya. Tena, usijifunze mambo mazuri tu ya hiyo biashara jaribu kudodosa na changamoto zake.
Ukipata bahati ya kushiriki kwenye hiyo biashara moja kwa moja kama kushinda hapo kwenye biashara ya mwenzako na kuona biashara ilivyo utaweza kujifunza mengi zaidi.
Wanaozifanya hizo biashara hata kama hawana elimu
kama ya kwako, ukikubali kushuka chini ujifunze kwao utagundua kuwa watu hawa huwa na vitu vingi sana vya kukufundisha walivyojifunza mtaani.
Nimeona baadhi ya wafanyakazi wenye biashara zao hata wakipita karibu na majirani zao kwenye biashara hawawasalimii. Usipozungumza na hawa watu ambao wao ndiyo huwa wanashinda huko sokoni, unategemea utawezaje kupata taarifa za yanayojiri mjini.
Kuna wakati inakubidi utumie hata fedha ili kufanya utafiti wa kina wa upatikanaji wa bidhaa, ufungashaji na upatikanaji wa masoko. Hii itakusaidia kupata picha halisi ya biashara unayotaka kwenda kuianzisha.
Kutokuwa na muda na biashara zao
Ni mara chache sana unaweza kumuachia uliyemuajiri asimamie biashara yako na akafanya kazi kama ambavyo unataka wewe. Ikitokea umepata mtu ambaye anaweza kusimamia biashara yako kama ambavyo ungefanya wewe, ni kwa bahati sana. Mara nyingi sana biashara ili ifanikiwe lazima mwenye biashara awe na muda nayo.
Utakayemuajiri hatawasikiliza na kuwajibu wateja kama ambavyo ungefanya wewe, wakati mwingine hatauza bidhaa kwa bei ambayo ungeuza wewe. Tena hatatuza fedha kwa makini kama ambavyo ungefanya wewe.
Hata kama umebanwa na kazi yako kama hauna muda na biashara utakayoianzisha ni bora usiianzishe.
Tenga muda hata wa jioni kwenda na wewe kukaa hapo kwenye hiyo biashara ujifunze na kuona mambo yanavyokwenda. Wakati mwingine ukiweza ukae siku nzima uwahudumie wateja, uwasimamie watenda kazi wako.
Ukiwa unatenga muda kwa ajili ya biashara yako itakusaidia wewe kuifahamu kwa undani, kujua aina ya wateja unaowahudumia na mahitaji yao, wakati mwingine utajua hata mambo ambayo yanafanyika wakati wewe haupo.
Imani potofu kuwa biashara ni rahisi
Mtazamo wa haraka haraka wa wafanyakazi wengi ni kuwa biashara sio ngumu sana. Hawajui kwamba biashara ina changamoto zake na ni safari inayohitaji juhudi na kujitoa.
Baadhi yao wanajua kuwa ina changamoto ila kiasi cha changamoto wanachokipimia ni kidogo kuliko changamoto halisi za kibiashara.
Wakati mwingine utawaona maofisa wa serikali wakidai tozo kubwa kwa biashara ndogo sana. Kwa harakaharaka ukisoma mtazamo wao utagundua hawajui mazingira halisi ya biashara.
Inawezekana ukaona matunda ya biashara yako kwa haraka ila mara nyingi sana inahitaji uwekezaji wa muda mrefu, uvumilivu na kujifunza. Ukweli ni kuwa wengi tunafanya biashara ili tupate faida, ila tatizo la waajiriwa ni imani kwamba watawekeza leo watapata faida kubwa kesho.
Faida ni zawadi aipatayo mfanyabiashara kwa kuweza kuvumilia, kutoa muda wake, na kutumia rasilimali alizo nazo vizuri kutoa huduma bora kwa jamii.
Maana yake ni kwamba kiasi cha uvumilivu, muda utakaoutumia na rasilimali zingine ndiyo vinavyoamua kiasi cha faida. Ukiongeza uvumilivu, ukiongeza muda unaoutumia kwenye bishara yako, ukiongeza mtaji na ujuzi wa biashara utaweza kuongeza faida.
Kusahau gharama ya kujifunza biashara
Ni uhalisia ya kwamba kila anayeanzisha biashara anatamani asipate hasara. Ila uhalisia mwingine pia ni kuwa hasara kwa baadhi ya nyakati kwenye biashara haziepukiki. Hasara ni ishara kwamba kuna jambo haukulifanya sahihi. Hii inaitwa gharama ya kujifunza.
Hasara huwa inakusababisha uanze kuitazama biashara yako kwa upya tena. Unaanza kujiuliza maswali ya kwanini ulipata hasara? Yawezekana eneo uliloanzisha biashara yako sio eneo sahihi, wateja hawana uhitaji mkubwa wa bidhaa unazouza, bei unayouza sio rafiki kwa aina ya wateja uliowalenga na mambo kama hayo. Maswali haya hukusababisha uanze kudodosa zaidi kwa watu wengine.
Hasara huwanyenyekeza wenye kiburi, huongeza ufanisi kwenye utoaji wa huduma na umaridadi kwenye utengenezaji wa bidhaa. Wateja huanza kupewa thamani inayostahili. Jambo la kuzingatia ni kwamba wafanyakazi wasikate tamaa wanapoanza biashara na kupata hasara. Hakuna sababu ya kuacha biashara na kugeukia maisha mengine.
Ni lazima kuelewa kwamba kila jambo zuri lina gharama zake. Fedha utakazozitoa na kuziwekeza ni gharama mojawapo, ila hasara iweke pia kwenye mpangilio wako. Isikukatishe tamaa. Jifunze na uitumie kama fursa kupiga hatua zaidi.
No comments:
Post a Comment